new_red KARIBU UPAKUE FOMU KWA MAHITAJI MBALIMBALI:new_red MAOMBI YA NAFASI KATIKA SHULE; new_redMirathi / Urithi na Kununua / Kuuza KIWANJA BOFYA HAPA KUZIPATA new_red
Jumuiya ya Uamsho wa Wakristo Tanzania (UWATA) ilianza siku nyingi miaka zaidi ya hamsini (50) iliyopita, lakini kwa sababu ya taratibu za kusajili kucheleweshwa ndipo kukapelekea kutofahamika na wanajamii wengi. Jumuiya ya Uamsho wa Wakristo Tanzania (UWATA) ni muungano wa wakristo toka madhehebu mbalimbali walioungana pamoja kwa njia ya kutubu dhambi na kuziacha.Mwanzoni mwanzilishi na aliyekuwa Mlezi wa wokovu huu ambao msingi wake ni wa mitume na manabii alibabaika kupata jina sahihi la kitu alichopewa (WOKOVU) na Mungu na alichokiamini ndipo kwa muda mrefu ilikuwa ikiitwa “NJIA HII, NJIA YA FURAHA” hadi jumuiya ilipopata usajili wa kudumu kwa jina tajwa hapo juu.
Mwombezi

MWANZILISHI NA ALIYEKUWA MLEZI WA JUMUIYA YA UWATA: MAREHEMU MZEE HARRISONI YESAYA MWAKISWALELE (1920-1991). ALITEMBEA NA YESU MUDA WOTE TANGU ALIPOTUBU NA HATIMAYE KUPUMZIKA KATIKA BWANA.

Mpendwa msomaji kitu chochote kinachoendelea hata kama ni kwa muda gani kina namna kilivyo anzishwa na mara nyingi anayeweza kusema kwa uhakika na ukweli ni mwanzilishi au waasisi wake.Kwa nafasi hii ni vizuri kupata maelezo ya mwanzilishi na aliyekuwa mlezi wa Uwata.Mwanzilishi wetu anaitwa HARRISON YESAYA MWAKISWALELE aliyezaliwa mwaka 1920.Yafuatayo ni sehemu ya maelezo yake kuhusu hatua alizopitia hadi kupata wokovu kama alivyoandika katika kitabu chake cha kwanza kiitwacho ”NILISUMBULIWA SANA LAKINI NAMSHUKURU MUNGU ALIYENIOKOKA” Miaka sita baada ya kuzaliwa, mama yangu alifariki dunia na mimi kupelekwa kwa bibi mzaa mama nilikopata mateso mengi sana. Nilipofikia umri wa kwenda shule nilijiunga na shule za misheni(mission) na kupata elimu ya kawaida na ya dini pia lakini havikunisaidia kuacha dhambi, niliendelea na mipango ya kumfahamu Mungu hasa kuanza kujisomea Biblia “Kitu ambacho nilikuwa na bidii nacho ni kusoma Biblia; nilisoma kuanzia kitabu cha Mwanzo mpaka Ufunuo wa Yohana, nilisoma kwa bidii sana pia nilipenda kuyaelewa yote niyasomayo. Lengo hasa nilitaka kujua ni kanisa lipi ambalo linafuata mafundisho ya Biblia.Nilifanikiwa kurudia mara tatu kuanzia kitabu cha Mwanzo mpaka Ufunuo wa Yohana”

Nalijua kuwa Mungu yupo tena ni Mtakatifu wala hapendi dhambi, pia nilijua kuwa moto wa mbinguni upo ambao ni Jehanamu ya moto. Zaidi nilijua ubaya wa dhambi kwa hiyo sikuipenda kabisa lakini nilijikuta natenda dhambi bila kupenda (Rumi 7:19-20). Baada ya kutenda dhambi sikuona furaha ndani yangu wala sikupata amani kabisa.Nilibaki najilaumu na kulialia tu kuwa kwa nini nafanya dhambi? Jambo hili la kuona uchungu wa dhambi ndilo hasa lililonifanya nipige magoti mara kwa mara nilipoomba mbele za Mungu; ingawa sisi Walutheri hatuna tabia ya kupiga magoti labda mmoja mmoja aliyefunuliwa kufanya hivyo.

Wakati wa vita kuu ya pili ya dunia ya mwaka 1939-1945 nilikuwako vitani tangu mwaka 1942, nilikuwa Madagaska baada ya Buruma kwa wa Japan. Nilifanya makosa ambayo baadaye yaliniletea shida kubwa sana ambayo sitaisahau maishani mwangu sijui pengine baada ya kufa, pengine ndipo sitakumbuka shida iliyonipata kwa kujitakia. Makosa yaliyoniletea shida ni haya:-

Ilikuwa mwaka 1944 nilikwenda nyumbani likizo toka vitani ndipo nilimwendea mganga aliyekaribu na nyumbani pangu anipe dawa ya kujikinga na wachawi; maana niliwaogopa sana Wanyasa,Wajaluo na Wakamba maana hawa walikuwa na madawa kweli na ndio nilioishi nao vitani.Baada ya kunywa tu dawa ile ndipo nikajikuta nakimbia usiku wakati wa kulala.Hata nilipolala mchana pia nilikurupuka na kupiga kelele sana maana niliona mambo ya ajabu. Nayo ni haya; naliona jeshi la watu wanakuja kuniua au kunizika nikiwa hai.
Siku moja wakati narudi vitani kutoka Dodoma kwenda Mwanza baada ya kutoka Tabora; nilikurupuka na makelele ya kutisha nikawaangukia watu waliolala chini nikiwa kwenye Treni.Treni za siku hizo zilikuwa na dari ambako watu walilala, nami ndimo nilikokuwa. Ugonjwa huu ulinitesa tangu mwaka 1944 hadi 1957; baada ya kutubu madawa yote na uzinzi,magendo, rushwa na hasira. Huko kulikuwa ndio kupona kwangu toka shida kuu iliyonitesa mno. Sifa kwa Yesu!!.
  • Kilio cha kumlilia Mungu hasa kilianza mwaka 1950.Nilikuwa namlalamikia Mungu, nikiomba hivi:
  • Kwa nini napenda kufanya dhambi ambayo siitaki?

Baada ya kubadilika kwa miaka miwili nikajikuta naomba hivi:

  • Nifanye nini ili nipate kushinda dhambi?

Baada ya mwaka mmoja kupita nikajikuta naomba hivi:

  • Bwana unionyeshe njia, Bwana unionyeshe njia
  • Ndipo siku moja nikasikia sauti ikiniambia mwambie Yesu dhambi zako. SIKUIACHIA NAFASI HII IPITE. (Isaya 43:25-26). Ndipo nikaanza kumweleza Bwana dhambi zote nilizozitenda. Baada ya kumweleza yote Bwana wangu niliposema Amen.Nikajikuta nina furaha ya ajabu ambayo sijaiona hata siku moja. Nikasikia sauti ikiniambia; UMESAMEHEWA!!!!
  • Siku ya pili nikasikia sauti ikiniambia nenda kawaage makahaba wote ulio tenda nao uzinzi na kurudisha ulivyodhulumu ,ndipo nikafanya hivyo, nikawaaga, nikarudisha, nao wote niliowaibia wengine waliniambia nilipe, wengine walinitangazia msamaha.Nilimshukuru Mungu kwa ukuu wake na rehema zake na huruma kwa wanadamu.
  • Huo ndio mwanzo wa kuokoka kwangu.
    • Haya kuishia hapo, ndipo siku iliyofuata nilisikia sauti ikisema una miungu; ndipo ikanionyesha madawa yangu ya unga, mizizi,hirizi tatu.Haya madawa yalikuwa ya kujikinga nisilogwe, mengine ya bahati, ya kupendwa na watu, ya kutafutia vyeo kazini na mengine mengi.Nikatii na saa ileile niliikusanya na kuitupa chooni hata zile za Hospitali kwa hofu nilizitupa zote.
    • Baadaye nikafunuliwa kuwa dawa za Hospitali siyo mbaya kama zilivyo za kienyeji ambazo zina mapepo ndani yake, kwa sababu ugunduzi wa dawa za kienyeji ni mapepo yanayoongoza kugundua na zile za Hospitali ni uvumbuzi wa kisayansi (Mhubiri 7:29).

    • Mpendwa msomaji kama umeweza kusoma hadi huo mstari hapo juu, naamini umepata mwanga wa namna ilivyo ngumu kufika Mbinguni, bahati mbaya sana hakuna njia ya mkato ila kutubu dhambi na kuziacha kama inavyosisitizwa katika (Mithali 28:13), na (2 Timotheo 2:19). Kama umeelewa na kuona kuwa na sababu za kusafiri kwenda Mbinguni ungali bado duniani kama Bibilia inavyotuandaa basi ungana nasi katika mmojawapo ya matawi yetu yaliyopo kila kona ya Tanzania na hata katika mataifa ya jirani,pengine waweza kuwa uliwahi kuungama dhambi lakini bado hujapata kuzishinda' basi ujue hukutubu kwa dhati toka moyoni na Yesu bado hajaingia ndani mwako, karibu kwetu utapata maelekezo sahihi jinsi ya kutubu kwa dhati na kupata ushindi.Kumbuka ukifa hakuna muda wa kutengeneza, komboa wakati!!!.
Kujiunga na jumuiya ya UWATA mtu halazimika kutubu dhambi na kuziacha kabisa,hatimaye kushiriki katika shughuli mbalimbali za jumuiya.Kutubu dhambi ni hatua ya kwanza inayotokana na mtu kutaabishwa, kuteswa na kusumbuliwa na dhambi hivyo kuwa na sababu ya kuziacha na kuwa huru kabisa kama neno la Mungu linenavyo katika (Yohana Mtakatifu 8:32) ' tena mtaifahamu kweli,nayo hiyo kweli itawaweka huru' ; kuacha dhambi ni hatua ya pili ya kuupata wokovu wa kweli uliojengwa katika misingi ya Mitume na Manabii maana neno la Mungu linasema: “Lakini msingi wa Mungu ulio imara umesimama,wenye muhuri hii, Bwana awajua walio wake. Na tena, Kila alitajaye jina la Bwana na auache uovu.” (2Timotheo 2:19).

Mpendwa msomaji wa historia hii, Mungu hapendi dhambi na mara zote tukiwa dhambini yeye hatuoni sisi wanadamu alio tuumba kwa mfano wake bali huona dhambi na hivyo kupelekea kuiangamiza dhambi iliyoshikamana pamoja na sisi. Mimi na wewe tuliumbwa kwa utukufu mwingi wa Mungu, na mwumbaji alitupenda sana hata kutupa ufahamu mwingi na mamlaka juu ya vyote alivyovifanya ,lakini sisi tumeishia kumwacha na kutenda tuyaonayo mema machoni petu, ndipo kwa neema yake akaamua kuturejesha kwake kupitia kifo cha aibu na cha ushindi cha mwanawe wa pekee YESU KRISTO msalabani. Leo hii mimi na wewe usomaye muda huu tuna mambo matatu tu tupaswayo kuzingatia kabla ya kifo kutukuta:
  • Kumwamini Yesu Kristo na kuzitubu dhambi zetu kwake ili atusamehe bure!!- elewa kuwa hakuna gharama utakazoingia wakati wa kutubu zaidi ya kuzichukia na kuziaibisha mbele ya mashahidi wengi
  • Kuziacha dhambi tulizosamehewa bila gharama!! –“Na tena, Kila alitajaye jina la Bwana na auache uovu.”(2 Timotheo 2:19b)
  • Kufuata misingi na maagizo ya WOKOVU kunakopelekea mwanadamu aliyeziacha dhambi (akitembea katika msamaha) kuwa mtauwa – Mtakatifu.

Leo hii UWATA imekua na kufikia hatua ya kuwa na matawi kila kona ya nchi yetu (Tanzania) na katika nchi mbalimbali kama Marekani, Australia, Uingereza, Burundi,Uganda, Kenya, Zambia n.k. Matawi karibu yote katika nchi hizo yamepata usajili wa kudumu. Jumuiya pia inatoa huduma za jamii kama elimu kuanzia hatua ya awali hadi sekondari na chuo; tafadhali tembelea "MIRADI" hapo juu upate taarifa zaidi.