UAMSHO WA WAKRISTO TANZANIA (UWATA)
Afichaye dhambi zake hatafanikiwa, Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema (Mith.28:13)

UINJILISTI

  • UINJILISTI WA NDANI YA KANISA

    Uamsho wa Wakristo Tanzania (UWATA) ni muunganiko wa wakristo toka madhehebu mbalimbali waliotubu na kuziacha dhambi. Kwa kuwa UWATA siyo dhehebu, basi ina utaratibu wake wa kuhudumia waumini hao kadri Mungu anavyojifunua kwa nyakati tofauti. Katika kipindi hiki Bwana ameendelea kuliimarisha kanisa lake kwa mikusanyiko iliyofanyika katika Kanda mbalimbali za UWATA nchi nzima. Ni jambo la kumshukuru Mungu anayetuhangaikia wakati wote. Kila mwana UWATA anahimizwa kuzingatia mafundisho hayo kwa kuwa watendaji na si wasikiaji tu'[" Lakini iweni watendaji wa Neno na wala si wasikiaji tu hali mkijidanganya nafsi zenu"] Yak 1:22, kadri yanavyofunuliwa ili kuzidi kuimarika katika Imani na kuuendeleza utakatifu ambao hakuna mtu atakayemwona Mungu asipokuwa nao ["Kwa maana imeandikwa, mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu"] 1 Pet 1:16.

  • Kuhusu uinjilishaji nje ya jumuiya, tunamshukuru Mungu wa Mbinguni watu wameendelea kuhubiriwa injili na mwana UWATA mmoja mmoja na kupelekea wanaotubu dhambi kuongezeka kwa nyakati mbalimbali. Aidha mikutano ya injili imeendelea kufanyika kila mwaka na hivi karibuni imefanyika katika eneo la mpakani mwa Tanzania na Kenya (Namanga) na Bwana Yesu kujiokolea waumini zaidi ya mia moja sifa kwa Bwana!! Mahubiri pia yalifanyika kwa njia ya Redio - KIZITO yenye masafa kwa maeneo ya mpakani mwa Kenya na Tanzania. Bwana Yesu aliponya wagonjwa walioshindikana katika mkutano huo wa Namanga. Kwaya na Wahubiri waliendeleza kazi ya uinjilisti kupitia nyumba kwa nyumba na makanisani na Bwana aliendelea kuokoa huko pia na idadi kamili kwa ujumla wake kufikia mia tatu na zaidi sifa kwa Bwana Yesu.
    Unaweza kufuatilia mafundisho ya Neno la Mungu kupitia mkutano wa Namanga na Arusha kwenye youtube kwa jina: 'MKUTANO WA INJILI WA UWATA HUKO NAMANGA, ARUSHA'

  • UWATA inayo studio ya kurekodi sauti na video inayosaidia kutangaza habari njema kwa njia ya uimbaji. Aidha mradi huu unaendeshwa na tawi la Bethania-Dar es salaam, Kanda ya Mashariki. Kwa maelezo zaidi tafadhali bonyeza hapa