UAMSHO WA WAKRISTO TANZANIA (UWATA)
Afichaye dhambi zake hatafanikiwa, Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema (Mith.28:13)

KUTUHUSU SISI

  • UAMSHO WA WAKRISTO TANZANIA (UWATA) NI NINI?

    Uamsho wa Wakristo Tanzania (UWATA)

    Ni muunganiko wa wakristo toka madhehebu mbalimbali waliotubu na kuziacha dhambi. UWATA ilianzishwa mwaka 1956 na kusajiliwa 11 Februari 1998 kwa cheti cha usajili namba SO.No. 9067 kwa mujibu wa sheria ya vyama, - The Societies Ordinance, 1954. UWATA ni jumuiya ya Kikristo inayowahubiri watu watubu dhambi na kuziacha na kuishi maisha ya kumpendeza Mungu ili mwisho wa maisha yao hapa duniani waweze kuingia Mbinguni. UWATA huwahubiri watu watubu, na baada ya hapo kuwasaidia kubadili mwenendo wao wa awali uwe mzuri, waishi katika jamii wakiwa raia wema.

    UWATA siyo dhehebu bali waumini wake huendelea kusali katika madhehebu yao ya awali kulingana na mafundisho ya Bwana wetu Yesu. UWATA hufanya ibada zake kila siku kulingana na ratiba na taratibu ilizojiwekea.

    UWATA inajishughulisha pia na miradi ya kijamii kama kujenga na kuendesha shule; hospitali, mashamba na miradi mingine ili kukidhi matakwa ya wanajumuiya wake na wanajamii kwa ujumla na pia kujiingizia kipato.

  • Mpendwa msomaji kitu chochote kinachoendelea hata kama ni kwa muda gani kina namna kilivyo anzishwa na mara nyingi anayeweza kusema kwa uhakika na ukweli ni mwanzilishi au waasisi wake.Kwa nafasi hii ni vizuri kupata maelezo ya mwanzilishi na aliyekuwa mlezi wa UWATA. Mwanzilishi wetu anaitwa HARRISON YESAYA MWAKISWALELE aliyezaliwa mwaka 1920.Yafuatayo ni sehemu ya maelezo yake kuhusu hatua alizopitia hadi kupata wokovu kama alivyoandika katika kitabu chake cha kwanza kiitwacho ”NILISUMBULIWA SANA LAKINI NAMSHUKURU MUNGU ALIYENIOKOA”

    Miaka sita baada ya kuzaliwa, mama yangu alifariki dunia na mimi kupelekwa kwa bibi mzaa mama nilikopata mateso mengi sana. Nilipofikia umri wa kwenda shule nilijiunga na shule za misheni(mission) na kupata elimu ya kawaida na ya dini pia lakini havikunisaidia kuacha dhambi, niliendelea na mipango ya kumfahamu Mungu hasa kuanza kujisomea Biblia

    Kitu ambacho nilikuwa na bidii nacho ni kusoma Biblia; nilisoma kuanzia kitabu cha Mwanzo mpaka Ufunuo wa Yohana, nilisoma kwa bidii sana pia nilipenda kuyaelewa yote niyasomayo. Lengo hasa nilitaka kujua ni kanisa lipi ambalo linafuata mafundisho ya Biblia.Nilifanikiwa kurudia mara tatu kuanzia kitabu cha Mwanzo mpaka Ufunuo wa Yohana”.


    Nalijua kuwa Mungu yupo tena ni Mtakatifu wala hapendi dhambi, pia nilijua kuwa moto wa mbinguni upo ambao ni Jehanamu ya moto. Zaidi nilijua ubaya wa dhambi kwa hiyo sikuipenda kabisa lakini nilijikuta natenda dhambi bila kupenda (Rumi 7:19-20)".

    Baada ya kutenda dhambi sikuona furaha ndani yangu wala sikupata amani kabisa.Nilibaki najilaumu na kulialia tu kuwa kwa nini nafanya dhambi? Jambo hili la kuona uchungu wa dhambi ndilo hasa lililonifanya nipige magoti mara kwa mara nilipoomba mbele za Mungu; ingawa sisi Walutheri hatuna tabia ya kupiga magoti labda mmoja mmoja aliyefunuliwa kufanya hivyo. Wakati wa vita kuu ya pili ya dunia ya mwaka 1939-1945 nilikuwako vitani tangu mwaka 1942, nilikuwa Madagaska baada ya Buruma kwa wa Japan. Nilifanya makosa ambayo baadaye yaliniletea shida kubwa sana ambayo sitaisahau maishani mwangu sijui pengine baada ya kufa, pengine ndipo sitakumbuka shida iliyonipata kwa kujitakia. Makosa yaliyoniletea shida ni haya:-

    Ilikuwa mwaka 1944 nilikwenda nyumbani likizo toka vitani ndipo nilimwendea mganga aliyekaribu na nyumbani pangu anipe dawa ya kujikinga na wachawi; maana niliwaogopa sana Wanyasa,Wajaluo na Wakamba maana hawa walikuwa na madawa kweli na ndio nilioishi nao vitani.Baada ya kunywa tu dawa ile ndipo nikajikuta nakimbia usiku wakati wa kulala.Hata nilipolala mchana pia nilikurupuka na kupiga kelele sana maana niliona mambo ya ajabu. Nayo ni haya; naliona jeshi la watu wanakuja kuniua au kunizika nikiwa hai.

  • Siku moja wakati narudi vitani kutoka Dodoma kwenda Mwanza baada ya kutoka Tabora; nilikurupuka na makelele ya kutisha nikawaangukia watu waliolala chini nikiwa kwenye Treni.Treni za siku hizo zilikuwa na dari ambako watu walilala, nami ndimo nilikokuwa. Ugonjwa huu ulinitesa tangu mwaka 1944 hadi 1957 nilipotubu rasmi madawa yote na uzinzi, magendo, rushwa na hasira. Huko kulikuwa ndio kupona kwangu toka shida kuu iliyonitesa mno. Sifa kwa Yesu!!.

    • Kilio cha kumlilia Mungu hasa kilianza mwaka 1950.Nilikuwa namlalamikia Mungu, nikiomba hivi:
    • Kwa nini napenda kufanya dhambi ambayo siitaki?

    Baada ya kubadilika kwa miaka miwili nikajikuta naomba hivi:

    • Nifanye nini ili nipate kushinda dhambi?

    Baada ya mwaka mmoja kupita nikajikuta naomba hivi:

    • Bwana unionyeshe njia, Bwana unionyeshe njia
    • Ndipo siku moja nikasikia sauti ikiniambia mwambie Yesu dhambi zako. SIKUIACHIA NAFASI HII IPITE. (Isaya 43:25-26). Ndipo nikaanza kumweleza Bwana dhambi zote nilizozitenda. Baada ya kumweleza yote Bwana wangu nakusema Ameni,Nikajikuta nina furaha ya ajabu ambayo sijaihisi hata siku moja. Nikasikia sauti ikiniambia; UMESAMEHEWA!!!!
    • Siku ya pili nikasikia sauti ikiniambia nenda kawaage makahaba wote ulio tenda nao uzinzi na kurudisha ulivyodhulumu ,ndipo nikafanya hivyo, nikawaaga, nikarudisha, nao wote niliowaibia wengine waliniambia nilipe, wengine walinitangazia msamaha.Nilimshukuru Mungu kwa ukuu wake na rehema zake na huruma kwa wanadamu.
    • HUO NDIYO MWANZO WA KUOKOKA KWANGU.
      • Haya kuishia hapo, ndipo siku iliyofuata nilisikia sauti ikisema una miungu; ndipo ikanionyesha madawa yangu ya unga, mizizi na hirizi tatu. Haya madawa yalikuwa ya kujikinga nisilogwe, mengine ya bahati, ya kupendwa na watu, ya kutafutia vyeo kazini na mengine mengi.Nikatii na saa ileile niliikusanya na kuitupa chooni hata zile za Hospitali kwa hofu nilizitupa zote.
      • Baadaye nikafunuliwa kuwa dawa za Hospitali siyo mbaya kama zilivyo za kienyeji ambazo zina mapepo ndani yake, kwa sababu ugunduzi wa dawa za kienyeji ni mapepo yanayoongoza kugundua na zile za Hospitali ni uvumbuzi wa kisayansi (Mhubiri 7:29).

      • Mpendwa msomaji kama umeweza kusoma hadi huo mstari hapo juu, naamini umepata mwanga wa namna ilivyo ngumu kufika Mbinguni, bahati mbaya sana hakuna njia ya mkato ila kutubu dhambi na kuziacha kama inavyosisitizwa katika (Mithali 28:13), na (2 Timotheo 2:19). Kama umeelewa na kuona kuwa na sababu za kusafiri kwenda Mbinguni ungali bado duniani kama Bibilia inavyotuandaa basi ungana nasi katika mmojawapo ya matawi yetu yaliyopo kila kona ya Tanzania na hata katika mataifa ya jirani,pengine waweza kuwa uliwahi kuungama dhambi lakini bado hujapata kuzishinda' basi ujue hukutubu kwa dhati toka moyoni na Yesu bado hajaingia ndani mwako, karibu kwetu utapata maelekezo sahihi jinsi ya kutubu kwa dhati na kupata ushindi.Kumbuka ukifa hakuna muda wa kutengeneza, komboa wakati!!!.

  • Utaratibu wa kujiunga:

    Utaratibu wa kuwa mwanajumuiya katika UWATA ni kwa njia ya kutubu dhambi moja baada ya nyingine na kuziacha. Mambo yafuatayo ni budi kufanyika wakati wa kujiunga:

    1. Mhusika kushuhudiwa au kuhubiriwa Neno la Mungu, kuelekezwa na kukubali kwa hiari yake mwenyewe kutubu dhambi moja baada ya nyingine na kisha kuziacha kabisa. Kushuhudiwa au kuhubiriwa Neno la Mungu kunalenga kutimiza matakwa ya Neno la Mungu la Yn 6:44-45.
    2. Njia nyingine ni mtu anasikia sauti ya Mungu kuwa nenda ukatubu UWATA;
    3. Mwingine anavutwa na nyimbo zinazoimbwa nyakati za ibada;
    4. Mwingine anavutwa na mwenendo mzuri wa mwana UWATA mmoja mmoja au wana UWATA kwa ujumla wao;
    5. mwingine yupo katika kumtafuta Mungu au kuutafuta wokovu wa kweli na kuja kwenye tawi la UWATA yeye mwenyewe;
    6. Mwingine anatendewa muujiza mfano wa kuponywa ugonjwa unaomsumbua kwa maombezi ya mwana/wana UWATA;
    7. Na/au njia nyingine yeyote inayokubalika katika UWATA ya kulisikia Neno la Mungu na kuja kutubu.


    Baada ya kutubu dhambi moja moja ataahidi mbele ya Yesu na mbele ya mashahidi wengi kuwa hatarudia dhambi alizotubu. Mashahidi ni wana UWATA na neno "wengi" ni kuwepo kwa mwana UWATA mmoja au zaidi wakati wa kutubu.

  • UWATA wakati huu imekua kiasi cha kuwa na matawi katika nchi mbalimbali; ikiwemo Marekani, Canada, Australia, Burundi, Rwanda, Uganda, Kenya, Zambia na Malawi .

    Kukua huko kwa UWATA kumechangiwa na utekelezaji wa malengo yafuatayo:



    1. Kuhubiri Neno la Mungu ulimwenguni kote ili kila aaminiye atubu dhambi na kuziacha hatimaye afike Mbinguni.
    2. Kukusanyika kila siku kujifunza Neno la Mungu na Kuomba.
    3. Kuombea watu wote, nchi na Serikali pamoja na viongozi wake.
    4. Kuombea viongozi wa makanisa yote.
    5. Kutoa huduma za kijamii kama vile Elimu, Afya na Utunzaji Mazingira.
    6. Kujishughulisha na shughuli za kiuchumi kama vile kilimo, biashara na viwanda.